4 Desemba 2025 - 22:24
Maadhimisho ya Kifo cha Bibi Fatima Umm ul-Banin (a.s)

Bibi Ummul-Baneen aliwapenda Ahlul-Bayt wa Mtume kuliko alivyowapenda wanawe mwenyewe. Alipopata habari za huzuni za Karbala, hakumuuliza kwanza kuhusu wanawe wanne, bali alisema: “Nijulisheni kuhusu Hussein.”

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Bibi Fatima Ummul Banin (sa) alikuwa mke mtukufu wa Imam Ali (a.s) na mama wa Abul-Fadhl al-Abbas, Mbeba Bendera wa Imam Hussain (a.s) katika uwanja wa vita wa Karbala. Maana ya jina “Ummul Baneen” ni “Mama wa wana”. Wana wake wote waliuawa shahidi pamoja na Imam Hussain (a.s) katika tukio la Karbala. Bibi Fatima Ummul-Banin alifariki dunia tarehe 13 Jamadi al-Thani, mwaka 64 Hijria, katika mji mtukufu wa Madina, na akazikwa katika makaburi mashuhuri ya Baqi.


Umm ul-Banin: Mama wa Wana Wake

Na: Huda Jawad

Katika historia yote ya Uislamu, ni wanawake wachache tu waliojitokeza kama vielelezo vya ukamilifu wa mwanamke katika nyanja zote halali za kijamii na kidini. Pamoja na wanawake wanne wakubwa wa ulimwengu — Bibi Maryam, Bibi Asiya, Bibi Khadija, na Bibi Fatima Zahra (a.s) — wapo pia wanawake wengine ambao bila wao, dini ya Uislamu ingekuwa katika hali ngumu sana.
Bibi Fatima, binti wa Hizam bin Khalid bin Rabi, anayejulikana zaidi kama Bibi Ummul-Baneen (a.s), yuko miongoni mwa wanawake wa Kiislamu waliotukuka zaidi na wachamungu hadi leo, na ataendelea kubaki hivyo kwa sababu ya ujasiri wake, uchamungu wake, na msimamo wake thabiti kwa Mtume (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt wake (a.s).
Maisha yake, pamoja na kuwa yeye pia alikuwa binadamu kama sisi waliokosea, yanatupa mafunzo mengi sana yanayoonyesha aina ya tabia na ikhlasi (uaminifu wa dhati) ambayo tunaweza kuifikia.

Kielelezo cha Ulezi Bora wa Mama

Abu Nasr Bukhari anasimulia kutoka kwa Mufadhal bin Umar kwamba Imam Ja‘far as-Sadiq (a.s) alisema:
“Inasimuliwa kuwa Amirul-Mu’minin Imam Ali (a.s) alimwomba ndugu yake Aqeel, aliyekuwa mtaalamu wa nasaba za Waarabu, amtafutie mwanamke kutoka familia ya mashujaa ili amwoe na azae naye mwana shujaa. Aqeel akasema: ‘Muoe Fatima al-Kilabiyah, kwa kuwa hakuna katika Waarabu walio mashujaa zaidi kuliko baba zake.’ Basi Imam Ali akamwoa.”

Inastaajabisha kufikiri kuwa, licha ya Imam Ali (a.s) kuwa Simba wa Mwenyezi Mungu na mshindi wa Khaybar, bado alisisitiza kumuoa mwanamke shujaa ili azae mwana shujaa. Hili linatufundisha kuwa katika malezi sahihi ya watoto, wazazi wote wawili wana mchango mkubwa katika kupandikiza ucha-Mungu na tabia njema.

Jina halisi la Bibi Ummul-Baneen lilikuwa Fatima, lakini alipoingia katika nyumba ya Imam Ali (a.s), aliomba aitwe Ummul-Baneen ili asiwakumbushe watoto jina la binti wa Mtume (Bibi Fatima Zahra) na kuwahuzunisha. Licha ya kuwa alikuwa bi harusi mchanga mwenye ndoto na matarajio yake, aliamua kuwa mtumishi wa mayatima wa Bibi Fatima Zahra. Kwa upande wao, watoto walimheshimu sana na kumpenda, wakimuita mama yao.

Hili ni funzo la kujitolea kwa pande zote mbili pale mtu anapoingia katika familia ambayo tayari ilishaundwa.

Ummul-Baneen maana yake ni “Mama wa Wana”, jina linalomfaa kwa kuwa yeye na Imam Ali walipata watoto wanne:
Uthman, Ja‘far, Abdullah, na Abul-Fadhl al-Abbas, Lango la Kukubalika Dua na Mwezi wa Bani Hashim (a.s).

Wana wake wote wanne walipigana kwa ujasiri bega kwa bega na Imam Hussain (a.s) siku ya Ashura. Aliwapandikiza ndani yao upendo na utiifu kwa Mtume na Ahlul-Bayt wake, kiasi cha kusimama imara hata walipokuwa wanajua kuwa wangekutana na kifo mbele ya jeshi kubwa la batili. Wanaume kama hawa hawawezi kulelewa isipokuwa na mama mwenye imani na ujasiri.

Utiifu Wake kwa Ahlul-Bayt (a.s)

Bibi Ummul-Baneen aliwapenda Ahlul-Bayt wa Mtume kuliko alivyowapenda wanawe mwenyewe. Alipopata habari za huzuni za Karbala, hakumuuliza kwanza kuhusu wanawe wanne, bali alisema:
“Nijulisheni kuhusu Hussein.”

Alipopata habari za kuuawa shahidi kwa Imam Hussain (a.s), alisema:
“Mishipa yote ya moyo wangu imekatika. Kila nilicho nacho chini ya mbingu hii kiko tayari kutolewa kafara kwa ajili ya Imam Hussain.”

Kwa hakika, tabia za wana wa Ummul-Baneen ni kioo cha utukufu wake. Cha kushangaza zaidi ni kwamba Bibi Ummul-Baneen alikuwa binamu wa Shimr, mmoja wa wauaji wa Imam Hussain. Wakati wa tukio la Karbala, Shimr alipaza sauti:
“Wako wapi wana wa dada yetu?”

Al-Abbas na ndugu zake wakatoka na kumuuliza atakacho. Shimr akasema:
“Enyi wana wa dada yangu! Mnapewa dhamana ya usalama.”
Wakajibu:
“Ole wako na usalama wako! Unatupatia usalama ilhali mwana wa Mtume hana usalama?”

Al-Abbas akapaza sauti:
“Mikono yako ikatwe! Huu ni usalama gani mbaya unayotuletea? Ewe adui wa Mwenyezi Mungu! Wataka tutoe kumsaliti ndugu yetu na kiongozi wetu Imam Hussain na kuwatii wana wa baba waliolaaniwa?”

Kumuenzi Imam Hussein (a.s)

Bibi Ummul-Baneen alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kuanzisha majlisi za maombolezo ya Imam Hussain. Imam Sadiq (a.s) anasimulia:
“Ummul-Baneen, mama wa ndugu wanne waliouawa shahidi, alikuwa akienda Baqi na kuomboleza kwa maneno yenye uchungu mkubwa. Watu walikusanyika kusikiliza. Siku moja hata Marwan bin Hakam alikuja na akalia.”

Pamoja na wanawake wengine wa Bani Hashim, aliigeuza Baqi kuwa Hussainiyya, kituo cha maombolezo ya Imam Hussain. Yeye ndiye anayehesabiwa kuwa mtu wa kwanza kutunga mashairi ya kuomboleza Karbala na mashahidi wake.

Moja ya mashairi yake mashuhuri ni haya:

Yule aliyeona ujasiri wa Abbas uwanjani
Na pamoja naye walikuwa wana wa Haidar shujaa
Nikasikia mikono yake ilikatwa na kichwa chake kujeruhiwa
Ewe Mola, mwana wangu aliangukaje bila mikono ya kujikinga?
Lau angekuwa na upanga mkononi
Hakuna ambaye angeweza kumsogelea
Msiniite tena Mama wa Wana
Jina hili hunikumbusha majasiri wangu
Wakati walipokuwa hai, nilikuwa Ummul-Baneen
Sasa nimewapoteza, jina hili halinifai
Walikuwa kama simba wanne
Waliolala baada ya kuutoa vichwa vyao
Yeyote aliyekutana nao vitani
Alianguka kama mvua
Laiti kungepatikana aliyeniambia
Mikono ya Abbas ilikatwa kwa ukatili mkubwa…

Miaka michache baada ya tukio la Karbala, Bibi Ummul-Baneen alifariki dunia tarehe 13 Jamadi al-Thani, 64 Hijria. Lakini majlisi na tamaduni za maombolezo alizoweka zimeendeleza hai kumbukumbu ya shahada ya Imam Hussain na Ahlul-Bayt, na ni wajibu wetu kuendeleza urithi huu na kuifanya Karbala iendelee kuishi mioyoni mwetu.


Marejeo (References):

1-Mulla Bashir Rahim: The History and Philosophy of Aza of Imam Hussain

2-Shaikh Abbas al-Qummi: Mafatih al-Jinan (tafsiri ya Kiurdu)

3-Shaikh Abbas al-Qummi: Nafasul Mahmum

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha